“TAQIYYA”

TAQIYYA
Maana ya Taqiyya, kama alivyo tafsiri Sahaba Abdullah ibn Abbas ni “Kusema kwa ulimi na hali moyo unatulia kwa imani”. Kwa hiyo, Taqiyya ni kuficha imani ndani ya moyo, na kutamka kwa ulimi yaliyo kinyume na ya moyoni.
Taz: Tafsirul Qurtubi, J. 4, Uk. 57

Kwakupata ufafanuzi katika somo hili, tumsikilize Imam Bukhari anasema: “Imepokewa kutoka kwa Abu Dardai anasema: ‘Hakika sisi wallahi tunawakenulia jamaa ili hali nyoyo zetu zinawalaani.”

Taz: Tafsir ibn Kathir J.1, Uk. 365

Safwatut Tafasir J.1, Uk.196

Abu Dardai anatufahamisha hapa yakuwa: Wao wanapojumuika na baadhi ya watu wasioafikiana nao katika jambo fulani, huchanganyika nao kwa bashashi kubwa kwa kicheko na kukenua mena kama kwamba wanakubaliana na yao. Kumbe ndani ya mioyo yao wanawalaani!!! Hii ndiyo Taqiyya tunayo izungumza hapa, na ndiyo Taqiyya aliyoisema Mwenyeezi Mungu: “Waumini wasiwafanye makafiri kuwa viongozi badala ya waumini. Na atakaefanya hivyo, basi hatakuwa na chochote kwa Mwenyeezi Mungu, isipokuwa kwa kujilinda nao sana” 3:28. Iliposemwa: “Na atakaefanya hivyo” maana yake: “Atakaewafanya makafiri kuwa viongozi wake” Mwenyeezi Mungu anamwambia: “Hatakuwa na chochote kwa Mwenyeezi Mungu”. Kwa mantiq hii, Mwislamu yeyote anayeongozwa na kafiri, hana chochote kwa Mwenyeezi Mungu. Mpaka hapa hukumu hii itawagusa Waislamu wengi sana! Lakini Alhamdulillah hali haiko hivyo, kwa sababu ibara katika Aya inaendelea kusema: “Isipokuwa kwa kujilinda nao sanasana”. Taqiyya imemuopoa Mwislamu katika hukumu aliyohukumiwa laiti isinge kuwapo Taqiyya.

Kwa ajili hii, sahaba Ammar bin Yasir alipoadhibiwa na makafiri, akauliwa mama yake, Sumayya, mbele ya macho yake baada ya kuteswa sana. Hilo halikutosha, akachukuliwa baba yake Yasir akawekwa mbele ya macho yake, akateswa sana hatimae akauliwa, kisha ndipo walipomgeukia naye Ammar, akapigwa na kuteswa, Ammari ndipo alipotamka neno la kufru. Alipofika kwa Mtume (s.a.w.) Ammar aliliya sana na kusema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu, nitauweka wapi uso wangu ili hali mimi nimesema neno chafu (la kufru) baada ya kuteswa sana, na kuniulia mbele ya macho yangu wazazi wangu wawili baba na mama!! Kabla Mtume (s.a.w.) hajasema lolote Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya: “Anayemkataa Mwenyeezi Mungu baada ya imani yake (ataadhibiwa adhabu kali) isipokuwa yule aliyelazimishwa hali moyo wake unatulia kwa imani 16:106. Mtume (s.a.w.) akamsomea Aya hii Ammar bin Yasir, kisha akamwambia: “Basi, kama watarudia (kukutesa) rudia (nawewekuwapa maneno ya kufru).

Taz: Tafsir Ibn Kathir J. 2 Uk. 609

Tafsirul Qurtubi J. 10 Uk. 180

Tafsirul Khaazin J. 4 Uk. 117

Tafsirul Maraghi J. 14 Uk. 146.

Hii ndiyo Taqiyya wanayoelekezwa waumini, kama ambavyo Taqiyya inamfikisha Mwislamu katika ngazi ya Uumini. Mwenyeezi Mungu anasema: “Na akasema mtu muumini aliyekuwa mmoja wa watu wa Firauni anayeficha imani yake, jee! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyeezi Mungu?? 40:28. Huyu bwana alionyesha ukafiri, akasihi pamoja najamaa yake Firauni, lakini kwa ndani alikuwa muumini kweli kweli, akatumia Taqiyya ili Firauni asimjue.

Mpenzi msomaji! Bila shaka umeona nafazi ya Taqiyya iliyo nayo katika Uislamu, umefahamu kuwa Taqiyya ni kiungo muhimu sana kati ya Islam na Mwislamu. Umesoma Aya zilizozungumza kuhusu Taqiyya umemuona Sahaba Ammar bin Yasir alivyowakejeli makafir kwa kutamka neno Ia kufru, kisha Mtume (s.a.w.) akaongeza kusema: “KAMA WATARUDIA NAWE RUDIA”.

WRITTEN BY: Taahir

No comments yet.

Leave a reply

Reset all fields