Darsa za mwezi wa Ramathan

Somo la kumi na nane (18)

Assalam alaikum

Katika darsa letu la leo tuta tazama baadhi ya hukumu nyeti zinazo ambatana na usiku wa mwezi wa Ramadhan. Tukizijua hukumu hizi swaumu zetu zitakuwa katika njia iliyo nyooka. Na kama hatutazijua hukumu hizi basi swaumu zetu zita haribika, itatubidi kulipa deni pamoja na kulipa kafara. Jambo ambalo ni kubwa sana!

Hebu na tutazame kwa ukaribu aya inayo ambatana na hukumu za usiku wa mwezi wa Ramadhan.

Mwenyezi Mungu anasema katika sura al Baqara, sura ya pili aya 187 kama ifuatavyo;

“Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha”

Aya hii ni ndefu na ina hukumu kadhaa ambazo ni muhimu kuzichambua kidogo kidogo na hatua kwa hatua. Insha Allah hilo tutalifanya katika darsa la leo na katika madarsa yanayokuja.

Kwa kiarabu aya hiyo inasomeka hivi;

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَكُمْ وَأَنْتُمْ لِبَاسٌ لَهُنَّ ۗ عَلِمَ اللَّهُ أَنَّكُمْ كُنْتُمْ تَخْتَانُونَ أَنْفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنْكُمْ ۖ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ ۚ وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنْتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ

Hebu na tuanze uchambuzi wa aya hii hatua kwa hatua;

1. Maingiliano ya kujinsia kati ya mume na mke

Katika dini ya Kiislamu hairuhusiwi kuwa na maingiliano kati ya mwanamume na mwanamke bila ya kuoana. Endapo watu wataamua kuwa na maingiliano hayo bila ya ndoa, hiyo ita itwa uzinifu au zinaa.

Na zinaa ni kitendo kibaya kabisa mtu kukifanya kwani kinaleta ufisadi wa hali ya juu katika jamii zetu. Madhara yake ni mengi na husababisha maafa makubwa. Na la muhimu zaidi ni kuwa zinaa inamchukiza sana Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam).

Maingiliano ya kijinsia kati ya mume na mke yanaruhusiwa baada ya ndoa, na yanaruhusiwa katika nyakati zote. Kuna wakati mke na mume hawaruhusiwi kukutana kimwili, ha haswa katika mchana wa mwezi wa Ramadhan.

Ama maingiliano hayo yameruhusiwa na Mola Mtukufu katika usiku wa Mwezi wa Ramadhan. Ruhusa hii imo ndani ya Qur’an.

Mwenyezi Mungu anasema;

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَكُمْ وَأَنْتُمْ لِبَاسٌ لَهُنَّ ۗ عَلِمَ اللَّهُ أَنَّكُمْ كُنْتُمْ تَخْتَانُونَ أَنْفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنْكُمْ ۖ

“Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni”

– Aya inazungumzia kuwa ni halali kwa mke na mume kuwa na maingiliano ya kijinsia katika usiku wa mwezi wa Ramadhan
– Wanawake ni sawa na vazi lenye kuwasitiri wanaume
– Wanaume nao ni sawa na vazi lenye kuwasitiri wanawake
– Mke na mume ni sitara ya kila mmoja. Sitara ya kutokufanya maaswiaya.
Sehemu ya pili ya aya hii inazungumzia historia na khalfia ya kuteremka kwake;
– Zamani maswahaba walizikhini nafsi zao kwa wake zao
– Mwenyezi Mungu akaleta hukumu hii ya ‘ruksa’
– Maswahaba wakaomba msamaha kwa kujihini huko
– Mwenyezi Mungu akawasamehe na kukubali toba yao

Ay hii hapa imezungumzia ruhusa ya kuwepo maingiliano ya kijinsia kati ya mume na mke katika usiku wa swaumu. Na neno ruhusa ni vizuri ieleweke kuwa halimaanishi lazima.

Ruhusa ya maingiliano kati ya mke na mume iko katika usiku wa mwezi wa Ramadhan, lakini si lazima kuwepo na maingiliano hayo. Hayo ni makubaliano kati ya wawili walio oana.

Maingiliano hayo ya kijinsia ni lazima yawe ndani ya usiku ili swaumu ipate kuwa sahihi.

Ni wajibu kwa mke na mume kuchunga kuwa jambo hilo linabaki katika wakati wa usiku. Sio baada ya alfajiri au mchana wa swaumu!

Ni lazima kuoga janaba baada ya maingiliano hayo, na kuoga huko kuwe ni ndani ya usiku huo huo!

Insha Allah tutaendela na darsa hili katika somo lijalo.

Ewe Allah tunakuomba utukubalie swaumu zetu. Tunakuomba utusamehe pale tulipokukosea. Jaalia mapenzi na masikilizano katika familia zetu. Wenye kutaka kuoa au kuolewa ya Rabbi wafanyie wepesi. Wajaalie wake au waume waliokuwa wema kwao. Ewe Mola tunakuomba vizazi vyetu vijaalie viwe vyema.

Amin Rabbal alamiin

Ndugu yenu
Ayub Rashid


Somo la kumi na tisa (19)

Assalam alaikum

Katika darsa lililopita tulitazama baadhi ya hukumu nyeti zinazo ambatana na usiku wa mwezi wa Ramadhan. tukatazama kwa ukaribu aya inayo ambatana na hukumu za usiku wa mwezi wa Ramadhan. Tulirejea katika sura al Baqara, sura ya pili aya 187, tukaona Mwenyezi Mungu anavyosema kama ifuatavyo;

“Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha”

Tukalizungumzia swala kubwa la

1. Maingiliano ya kujinsia kati ya mume na mke katika usiku wa mwezi wa Ramadhan.

Tukamalizia kwa kusema kuwa Maingiliano hayo ya kijinsia ni lazima yawe ndani ya usiku ili swaumu ipate kuwa sahihi. Na pia ni wajibu kwa mke na mume kuchunga kuwa jambo hilo linabaki katika wakati wa usiku. Sio baada ya alfajiri au mchana wa swaumu! Na kwamba ni lazima kuoga janaba baada ya maingiliano hayo, na kuoga huko kuwe ni ndani ya usiku huo huo!

Kwa kuwa aya tunayoitazama ina hukumu nyingi za kuziangalia kwa ukaribu, leo wacha tutazama kipengee hiki kisemacho ndani ya aya hii
“Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku”
Sura al Baqara, sura ya pili aya ya 187

Hapa katika sehemu hii Mola wetu mlezi anatupa ruhusa ya kula na kunywa katika usiku wa mwezi wa Ramadhan. Na kwamba ruhusa ipo kulifanya kila jambo lililokuwa likifungulisha swaumu linaruhusiwa kulifanya ndani ya usiku. Mradi lisiwe la maaswiya.

Maswala muhimu

Aya inazungumza kuwa swaumu ina anza weupe wa alfajiri unapo anza mpaka weusi wa usiku unapo ingia! Hebu tupazingatie hapo!

Kwa maneno yetu tulilyoyazoea, swaumu ina anza alfajiri mpaka magharibi. Hapa Mola wetu anasema kuwa swaumu ina anza weupe wa alfajiri unapo anza mpaka weusi wa usiku unapo ingia! Je makusudio ni nini?

Ni kwli kuwa kufunga swaumu kuna anza pale afajiri ya kweli inapokuwa imeingia. Hapo ndipo tunapoanza kujizuia kula na kunywa. Ni katika wakati huo ndio adhana ya swalatul Fajri inapo adhiniwa. Kwa wengine wetu huita hii adhana ya pili. Ni wakati huo ndio unaoitwa kwa Kiingereza kama ‘dawn’, kwa kiarabu ‘Fajr’ na Kiswahili cha Kiislamu wakati wa swala ya alfajiri. Sio kila alfajiri!

Endapo mtu atakula na kunywa na mara akaisikia adhana ya alfajiri ikiadhiniwa, atatakiwa kuwacha kula na kunywa mara moja. Na kama kuna chakula mdomoni, basi itamlazimu akiteme! Kwani kula baada ya wakati umeingia utaifanya swaumu ya siku hiyo iharibike na ije ilipwe pamoja na kutoa kafara!

Ikiwa mtu atakula na kunywa bila ya kujua kuwa wakati wa alfajiri umeingia, na au akaamini kuwa muda wa kula bado hauja isha, kisha ikaja ikambainikia kuwa amekula baada ya alfajiri kuwa imeshaingia, swaumu yake mtu huyo itakuwa sahihi. Ataendelea kufunga kama kawaida. Ila ni vizuri baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhan aje ailipe siku hiyo.

Swaumu huendelea tangu alfajiri mpaka magharibi. Je magharibi kisheria ni wakati gani?

Kuna maoni ya aina mbili;

1. Magharibi huwa ni pale mara tu jua linapo zama

2. Magharibi huwa baada ya kuzama jua na kupotea mawingu mekundu yanayo onekana upande wa mashariki.

Tofauti ya maelezo hayo inatokana na ufahamu wa aya hiyo hapo juu, na haswa sehemu isemayo “ … Kisha timizeni Saumu mpaka usiku…”.

Je, magharibi ni mgharibi kwa maana ya baada tu ya kuzama jua? Au magahribi ni magharibi baada ya kuzama jua na kuwa usiku?

Wataalamu wa mambo ya sheria ya Kiislamu wametofautiana kuhusu swala hilo.
Ndio maana utaona adhana za magharibi huwa zinatofautiana kiasi Fulani. Baadhi ya adhana husikika mara tu jua linapozama, na nyingine husikika kama baada ya dakika kumi baada ya zile za kwanza.

Cha muhimu katika swala hili ni kuwa na uhakika wa kuwa magharibi imeingia na ndipo mtu aweze kufungua swaumu yake. Kwani kuna hatari kubwa kama mtu atakuwa amefunga mchana kutwa na kisha afungue kabla ya wakati kutimia.

Tunamuomba Allah atukubalie swaumu zetu na atujaalie tuwe katika orodha ya waliofunga kisawa sawa.

Amin Rabbal alamiin
Ndugu yenu
Ayub Rashid


Somo la ishirini (20)

Assalam alaikum
Katika darsa lililopita tulitazama kuhusu swala la kuanza na kumaliza kufunga. Tulitazama maana ya alfajiri na magharibi.
Tulihitisha somo letu kwa kuutazama umuhimu wa kuwa na uhakika wa nyakati hizo mbili kuwa zimetimia, nazo ni fajri na magharibi.

Leo tunataka insha Allah, kutazama swala la kukaa itikafu. Nini maana ya itikafu? Itikafu hukaliwa wapi? Nini umuhimu wa itikafu na ni nini chanzo cha ibada hii ya itikafu? Na ni zipi hukumu zinazo ambatana na ibada hii muhimu ya itikafu?

Maana ya itikafu
Itikafu ni kukaa msikitini kwa ajili ya kufanya ibada.
Ibada hii ni ya sunna wala si faradhi. Ni ibada ya sunna iliyotiliwa mkazo.

Itikafu hukaliwa wapi?
Ibada hii hukaliwa msikitini, na huwa katika msikiti unaoswaliwa. Na sio nyumbani au mahala pengine popote.

Itikafu hufanywa kwa kukaa msikitini kwa muda wa siku tatu, kama walivyokuwa watu wa Madina wakifanya. Wengine wana maoni tafauti.
Ibada hii hufanywa wakati mtu akiwa amefunga.

Mwanamke anaweza kukaa itikafu msikitini. Baadhi ya maulamaa wa Kiislamu wamesema kuwa ni bora kwa mwanamke kukaa kwake kuwe ni nyumbani kwake.

Umuhimu wa itikafu
Faida ya ibada hii ni nyingi, miongoni mwazo ni;
– Kuwa karibu na Muumba wetu kwa kumuelekea yeye tu
– Kuihuisha sunna ya Mtume wetu na maswahaba wake
– Kujitenga na hii dunia na harakati zake kwa kukaa msikitini
– Kuzisafisha roho zetu kwa ibada mbali mbali
– Kujishughulisha kwa jambo moja tu la ibada
– Kujumuika na watu wengine wenye malengo mamoja katika ibada hii

Chanzo cha Itikafu
Qur’an tukufu imeitaja ibada hii katika Sura al Baqara, sura ya pili, katikati ya aya ya 187. Asili ya ibada hii inatokana na mafunzo ya Mtume (swallahu alaihi wa aalihi wa sallam), na kwamba maswahaba walifundishwa kukaa katika ibada ya itikafu.
Baadhi ya hukumu zaitikafu
– Itikafu inatakiwa kukaliwa msikitini, msikiti ambao unaoswaliwa. Sio katika ukumbi au uwanja, na kadhalika.
– Itikafu sahihi ina ambatana na swaumu. Yaani mtu anapotaka kukaa itikafu basi awe amefunga.
– Muda wa itikafu sahihi ni chini ya siku tatu. Zinaweza zikawa zaidi ya hizo.
– Wanaume na wanawake wanaokaa itikafu hawatakiwi kuwa katika mahusiano ya kijinsia, kwa kipindi chote cha itikafu.
– Mtu anaekaa itikafu hatakiwi kutoka toka nje ya msikiti bila ya kuwa na dharura. Anaruhusiwa kutoka kwa ajili ya kwenda kuoga na kutawadha na kujisaidia.
– Waati wa kukaa itikafu haitakiwi kujishughulisha na maswala ya dunia na kuyafuatilia kwa ukaribu.

Faida, Hekima na busara ya ibada hii
Watu wengi leo duniani tukiwemo sisi waisilamu, tumejishughulisha sana na na ulimwengu huu. Na mara nyingi huwa hatupati furs ya kuwa na mazingatio mazuri katika ibada zetu. Concentration yetu inakuwa ndogo katika ibada kwa sababu ya aina ya maisha ya haraka tunayoishi leo.
Kwa upande mwingine tumeshughulishwa na habari za ulimwengu, habari za michezo, simu za mikononi na mengineyo mengi yasiokuwa na umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kiroho.
Ibada ya Itikafu kaileta kwetu Mwenyezi Mungu ili itufae sisi kwa kuleta mapumziko katika maisha yetu. We need a break! Pindi tutakapo amua kujipumzisha kwa muda na yote yanayotushughulisha na dunia na tuka amua kuwa na mazingatio katika ibada zetu, maisha yetu yatakuwa na muelekeo mzuri na nafsi zetu zitatulia badala ya kuhaha huku na kule.
Enapo tutafikia hapo tutaweza kuzitambua neema nyingi alizotuneemesha Allah na kupata furs ya kusema kwa dhati Alhamdulillah kwa kila neema ambayo tulikuwa tumeisahau.

Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa sisi kurudi kwa Mola wetu kwa ibada mbali mbali, na miongoni mwa ibada hizo ni kukaa itikafu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie tuweze kupata fursa ya kukaa itikafu. Allah atujaalie tuweze kuwa na mazingatio katika ibada zetu.

Ndugu yenu
Ayub Rashid


Somo la ishirini na moja (21)

Assalam alaikum

Katika darsa la leo tunakusudia kuzungumzia juu ya sunna muhimu ya Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam). Sunna hii au kitendo muhimu alichokuwa akipenda kukifanya katika usiku wa mwezi wa Ramadhan. Sunna hii si nyingine bali ni kula daku.

Daku katika lugha ya kiarabau inajulikana kama suhuur. Neno suhuur lina fungamana na wakati kabla ya kuingia swala ya alfajiri.
Wakati huo kwa kiarabu unajulikana kama sahar au as-haar. Kwa hivyo ukisikia suhuur kumbuka sahar=suhuur ni daku na sahar ni wakati wa kula daku.

Lugha nyingine huiita daku kama seher au sehri. Na endapo utakuwa na kalenda inayozungumzia nyakati za saa za swala, futari na wakati wa mwisho wa kula daku utakutana na maneno kama hayo.

Sunna ya Mtume (swallallahu alahi wa aalihi wa sallam) ilikuwa ni kuchelewesha kula daku. Na imepokewa katika Hadith kuashiria kuwa ni vizuri kuchelewesha kula daku.

Na tunapozungumzia sunna ya Mtume, ni muhimu sana kuelewa katika ufahamu wake hapa kuwa sunna ni jambo linalopendeza kufanywa. Ukilifanya utapata thawabu, na usipolifanya hutopata thawabu wala madhambi.

Jambo ambalo ni sunna linapendeza kufanywa. Lakini si lazima kulifanya.

Tukirudi katika suala letu la kula daku, tutafahamu kuwa kula daku ni sunna. Ukila daku kama ni sunna utapata thawabu, na usipokula daku hautopata thawabu wala hutopata dhambi. Lakini ni vizuri ujue kuwa kula daku si lazima!

Kwa hivyo ukikosa kula daku kwa kupitiwa na usingizi usije ukakosa kufunga! Kwani kufunga mwezi wa Ramadhan ni wajibu na kula daku ni sunna. La wajibu ni lazima kulifanya na la sunna ni vizuri kulifanya!

Je, daku ni kula chakula gani?

Katika Hadith nyingi zinazoelezea sunna ya Mtume (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam) zinataja kuwa yeye kipenzi chetu alisema kuwa daku ni kula japo tende moja na au kunywa funda la maji.

Maelezo hayo yanatujulisha kuwa kula daku si lazima kula chakula Fulani kila usiku wa mwezi wa Ramadhan. Kama baadhi ya watu wanavyo dhania kuwa daku ni lazima iwe ni wali kwa mchuzi, au pilau kwa kachumbari, na au sima au ugali kwa mboga za majani au chai ya maziwa kwa mandazi, na au mfano wa hayo!

Tukizingatia katika swala zima la daku ni kuwa mfungaji anatakiwa kuifanya daku kuwa ni ibada na sio ada.
Ibada Kwa maana ya kuwa unapo amka usiku na kuamua kula daku kwa ajili ya kufunga kesho yake, basi jikurubishe kwa Mola wako kwa kula chochote utakacho amua kula kwa kiasi kidogo na kwa kufuata sunna ya Mtume wetu, alaihi salamullah. Amani ya Mola iwe juu yake.

Daku ni kama futari, katika kula daku kula chochote na kunywa kinywaji chochote ili uianze siku yako kwa kutia kitu kidogo tumboni.
Na futari nayo ni kula chakula chochote kwa ajili ya kufungua swaumu yako, na si lazima kuwa futari ni sharti iwe ni mihogo kwa samaki na mfano wake.
Cha muhimu katika mwezi wa Ramadhan ni kutenga muda mwingi kwa ajili ya ibada ya swala, dua na kusoma Qur’an na na ibada nyingine. Na sio kuutenga muda mwingi kwa ajili ya kula aina kwa aina mbali mbali za chakula katika daku na futari.

Na wala huu si mwezi wa kupika sana na kisha kutupa vyakula katika majalala, na hivyo kuingia katika dhambi kubwa sana ya kufanya israfu. Hilo halimpendezi kabisa Mola wetu, na huenda likatusababishia ufakiri.

Mola atuwezeshe kubadilisha nyendo zetu katika mwezi huu Mtukufu.
Na atujaalie tuweze kufikia kiwango cha juu cha ibada zetu, amin.

Ndugu yenu
Ayub Rashid


Somo la ishirini na mbili (22)

Assalam alaikum

Swala za faradhi tunazo ziswali kila siku ni tano, kama sote tujuavyo. Swala hizi tano zina rakaa kumi na saba. Katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan huwa waisilamu wengi wakiswali mbali na swala za faradhi,huwa wakiswali swala za sunna.

Katika somo la leo insha Allah tutazungumzia kuhusu swala za sunna zinazo swaliwa katika mwezi wa Ramadhan.

Mwezi wa Ramadhan umejaa Baraka zake nyingi, na miongoni mwazo ni kuwaona watu wakijishughulisha na ibada mbali mbali, na kilele cha ibada hizo ni swala.

Kuswali swala tano za faradhi ni wajibu na ni nguzo kubwa katika nguzo za Uisilamu.
Imepokewa katika Hadith ya Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema;

“swala ni nguzo ya dini, yeyote atakae isimamisha nguzo hii atakuwa ameisimamisha dini, na yeyote atakaeivunja nguzo hii atakuwa ameivunja dini”

Na katika Hadith za Mtume Muhammad (ishuke juu yake rehema na juu ya jamaa zake) amepokelewa akisema kuwa;

“Swala ni nguzo ya dini, ikiwa swala itakubaliwa, basi na ibada nyingine nazo zitakubaliwa, na ikiwa swala itakataliwa, basi na ibada nyingine nazo Pia zita kataliwa”

Bila shaka yoyote Hadith hizo zina ashiria na kusisitiza umuhimu wa swala tano za faradhi za kila usiku na mchana.

Swala za sunna au za mustahab

Kuna swala nyingine ambazo mja wa Mwenyezi Mungu anasisitiziwa kuziswali.
Swala hizi hujulikana kama swala za sunna au swala za mustahab au mustahabbaat.
Swala hizi si za lazima lakini zikiswaliwa humpelekea mtu kulipwa ujira mkubwa. Humletea mtu mafanikio mengi na humfanya mtu apendwe na Mola wake Mtukufu. Na dua zake zipate kukubaliwa.

Hebu fikiria, ukiwa utaenda dukani au sokoni kunua bidhaa fulani, ukalipa pesa za bidhaa ile kwa mujibu wa makubaliano. Mara baada ya kulipa pesa hizo, muuzaji akaamua kukuongezea bidhaa nyingine ya bure, namna gani utafurahi kwa kupewa nyongeza hiyo ya bure.!
Sasa hebu rudi katika maudhui yetu ya swala, sisi tunaposwali swala za faradhi huwa tumetekeleza wajibu wetu kwa Mola wetu, na kama tutaswali swala za sunna au za mustahab, tutakuwa tumemfanya Mwenyezi Mungu avifurahie vitendo vyetu, sasa hebu fikiria furaha yake kwetu itakuwa na malipo kiasi gani?!

Menyezi Mungu anasema katika suratul Baqara, sura ya pili aya ya 184

“…Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake…”

Kuna aina nyingi ya swala za sunna/mustahab ambazo huswaliwa kila siku; kwa mfano, ni sunna kuswali rakaa mbili kabla ya kuswali swala ya alfajiri. Na ni sunna kabla ya kuswali adhuhuri kuswali rakaa mbili, kisha ukatoa salam, na kisha ukaswali rakaa nyingine mbili, ukatoa salam, na kisha nyingine mbili tena, ukatoa salam, na ukamalizia rakaa nyingine mbili kisha ukatoa salam. Jumla ya rakaa hizo huwa ni nane. Na pia ni sunna kabla ya alasiri kuswali rakaa nane kama ulivyofanya kabla ya adhuhuri.

Ama baada ya swala ya magharibi, ni sunna kuswali rakaa mbili kisha ukatoa salam, na kisha kuswali rakaa mbili nyingine na kisha kutoa salam. Jumla ya rakaa hizo huwa ni nane. Na amma baada ya swala ya Isha ni sunna/mustahab kuswali rakaa moja ukiwa umesimama. Na kama utataka kuswali ukiwa umekaa basi utaswali rakaa mbili.

Ni sunna iliyotiliwa mkazo sana kuswali rakaa kumi na moja (11) za swala ya usiku. Swalatu Layli, au kisimamo cha usiku.
Hizi huswaliwa rakaa mbili mbili mara tano kwa salam na kisha kumalizia na rakaa moja. Kwa kifupi huwa hivi; 2+2+2+2+2+1=(11).

Swala hizi za usiku Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam) alikuwa haziwachi kuziswali.

Siku zote alikuwa akiamka kabla ya alfajiri na kujitengea muda maalum wa kuziswali swala hizi za usiku. Swala hizi zenye rakaa kumi na moja zimegawanyika katika makundi matatu; kundi la kwanza ni rakaa nane (8), kundi la pili ni rakaa mbili (2), hizi mbili zinajulikana kama za Shuf’aa, na kundi la mwisho ni rakaa moja (1), hii inajulikana kama witri.

Endapo mtu atashindwa kuswali zote kumi na moja kwa sababu zozote zile, basi na asikose kuswali rakaa mbili za shuf’aa na moja ya witri (2+1).

Swala hizi za usiku zina siri kubwa ya kupatikana mafanikio katika maisha yetu.

Qur’an tukufu imezitaja swala hizi za usiku katika sura ya al Israa ambayo pia inajulikana kama sura Bani Israil, sura ya 17, aya ya 79 kama ifuatavyo;

“Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika”

Kama Mtume wetu Mtukufu alinyanyuliwa daraja kwa sababu nyingi na moja wapo ni swala za usiku, basi na yeye katupendela kheri kwa kutusisitizia kuswali swala za usiku. Swalatul layli, qiyamul layl, au Tahajjud ndivyo zinavyojulikana.

Watu wengi huswali tarawehe kama swala za sunna na huziswali swala hizi baada ya swala ya Isha.
Kwa hakika ilivyo bora, na kama alivyosema khalifa wa pili Umar bin al Khatwabi, ambaye yeye ndiye muanzilishi wa swala hii kwa mujibu wa inavyoswaliwa sasa hivi duniani. Alipokelewa akisema kuwa atakaeswali mwisho wa usiku ni bora kuliko yule atakaeswali mwanzo wa usiku. Ni bora basi mtu akaswali swala za usiku, akiwa peke yake na Mola wake, kwani uzito wake umeelezwa katika Qur’an (17:79) na pia katika Hadith za Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam).

Tuna muomba Mola wetu atujaalie tuwe ni wenye kusimamisha swala. Atujaalie Mola wetu tuwe ni wenye kupenda kuswali swala za Sunna na Mustahab. Ya Rabbi tukubale swala zetu, ya Rabbi tukubalie swala zetu, ya Rabbi tukubalie swala zetu.
Amiin, Rabbala alamiin.


Somo la 23

Assalam alaikum
Darsa letu la leo litazungumzia kuhusu sunna ya kufuturisha. Umuhimu wa kufuturisha na jinsi sunna hii inavyoleta uhusiano mzuri katika jamii.
Kuwafuturisha watu wengine ni moja katika mambo yanayoleta furaha katika jamii na yenye kumletea mtoa futari utulivu wa moyo na thawabu kubwa kutoka kwa Mola wake.
Mtume wetu Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa salaam) ameisisitiza sana sunna hii ya kuwafuturisha wengine waliofunga. Kwa mfano katika khutbah yake ya kuwa andaa maswahaba wake na funga ya Ramadhan aliwaambia;
“man Fattwara minkum swaaiman mu’minan kaana Kaman a’ataqa raqabah”, akimaanisha kuwa ‘yeyeote miongoni mwenu atakaemfuturisha mtu mu’min aliyefunga atakuwa sawa na Yule aliyemuwacha huru mtumwa’.
Kwa hakika si rahisi kumuwacha mtumwa huru katika zama ambazo watu walipokuwa wakimiliki watumwa kama wafanya kazi wao. Kwa sababu watumwa walikuwa ni sawa na mashine za kufanyia kazi. Sasa kwa mtu ambae alikuwa akiwategemea watumwa wamfanyie kazi zake, aje amuwache huru mtumwa, na asiwe nae tena kama mfanya kazi wake, hilo halikuwa rahisi kabisa kutekelezwa.
Kwa hekima ya Mtume na mwendo wake mwema ulioambatana na ubinadamu wa hali ya juu na uliosimamia misingi ya Qur’an, alikuwa akiwasisitizia watu kuwaacha huru watumwa na akilisisitiza swala hilo katika misemo yake.
Katika Hadith yake hapo juu Mtume anafananisha swala la kumfuturisha mu’min na kumuwacha huru mtumwa,na kuonyesha umuhimu wa kujitolea kwa ajili ya kumridhisha Mola wetu Mtukufu.
Ni swala la kweli kabisa kuwa wapo baadhi ndogo ya waisilamu ambao pamoja na kuwa wana uwezo wa kuwafuturisha wenzao waliofunga, lakini kwa kuwa kufuturisha ni swala la kujitolelea, wao huona ni mzigo mkubwa sana kufanya hivyo, na wakabaki wakijilia wenyewe majumbani mwao peke yao. Na wakakosa kuifanyia kazi sunna hii muhimu.
Sunna ya kufuturisha
Mtume ameihimiza sunna hii ya kufuturisha katika Hadith yake alipokuwa akisisitiza swala hili, baadhi ya maswahaba walisema kuwa si kila mtu ana uwezo wa kutoa futari. Mtume (swallalhu alaihi wa aalihi wa sallam) aliwajibu kwa kusema ; muogopeni Allah, futurisheni japo ni kwa kutoa kikombe cha maji, mcheni Allah japo ni kwa kutoa nusu ya tende!
Nini kitolewe kwa ajili ya kufuturisha?
Mtu yeyote anaetaka kuwafuturisha wengine na aamue yeye njia bora ya kuwafuturisha wengine. Wapo baadhi ya watu hupenda kununua vyakula ambavyo bado havijapikwa na kuvigawa kwa wenye haja ili iwe ni futari yao. Na wap wengine ambao huamua kupikisha chakula na kukigawa kama futari. Na wapo wengine ambao huamua kutoa pesa na kuwapatia wenye haja. Njia zote hizo ni nzuri, ila tu ni vizuri kuchunga mwendo wa jamii mtu anayotaka kusaidia ili aende kwa mujibu wa maadili ya sehemu hiyo.
Wapo wengine ambao huamua kuwaalika wageni majumbani mwao ili wapate kufuturu pamoja nao. Njia hii pia ni nzuri, ila tu panatakiwa mualikaji achunge kuto kuwavunjia heshima na kuwadharau wale anaowaalika nyumbani kwake. Na asialike kundi moja tu la watu, bali ajitahidi kuwaalika watu wa matabaka mbali mbali katika jamii.
Maadili mema katika kufuturisha
Endapo tuta amua kuwaalika watu waliofunga majumbani mwetu, ni lazima tukachunga murua wa Kiislamu katika adabu za kumkirimu mgeni, kwani mgeni ana haki zake nyingi katika dini ya Kiislamu. Moja katika maadili hayo ni kumfaya mgeni ahisi ameheshimiwa. Itakuwa si sawa hata kidogo kumdharau mgeni wako kwa kumfanya ahisi amedharauliwa. Hiyo ni dhambi. Kwa mfano kumualika mgeni kwa futari na kumlisha chakula kilichobaki jana, na kumlisha makombo. Ikiwa hiyo ndiyo nia ya kumualika mgeni kula futari, basi hapo hapatakuwa na thawabu, bali patakuwa na ‘iqabu’ au dhambi. Ili tuyapate mafanikio na radhi za Allah ni lazima tuwafuturishe wengine chakula kizuri na fresh. Na tutoe kile ambacho sisi pia tutapenda kulishwa kama tutakuwa tumealikwa.
Na pindi tutakapokuwa tumealikwa majumbani mwa watu kwa futari, ni lazima tuchunge maadili ya ugeni. Tuende katika majumba ya watu kwa kufuatia kile kilichotupeleka huko tu.
Mwenyezi Mungu anatujulisha namna gani familia ya Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam) ilivyokuwa imefunga kwa muda wa siku tatu, walikuwa wamefunga swaumu ya nadhiri. Walipokuwa wameketi siku ya kwanza kufuturu walisikia mtu ana gonga mlango, walipomfungulia akasema yeye ni masikini na ana njaa na hana kitu cha kula. Wakampa futari yao na wao wakanywa maji tu. Kesho yake wakaendelea na swaumu ya siku ya pili. Na siku hiyo nayo walipokuwa wameketi tayari kufuturu mikate michache waliyokuwa nayo, wakasikia mtu akigonga mlango, walipomfungulia akasema yeye ni yatima, na hana chakula na ana njaa. Wakampatia kile walichokuwa nacho, wakanywa maji na kulalia swaumu yao ya siku ya tatu. Ilipofika magharibi ya siku ya tatu wakiwa wameketi kufuturu, wakasikia mlango ukigongwa. Walipofungua wakamuona mtu, akasema kuwa yeye ni mateka wa vita aliyeachiwa huru, ana njaa na hana kitu cha kula. Wakampatia chakula chao cha futari, na wao wakanywa maji. Mwenyezi Mungua akateremsha aya zifuatazo zilizomo katika sura ad Dahr, pia inajulikana kama sura al Insaan, sura ya 76 aya ya 7-9 kuwasifu.
“Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana. Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.Hakika sisi tunakulisheni kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani”
Mwenyezi Mungu aliwalipa malipo makubwa waja hao wema, ambao walikuwa ni Fatima binti Rasulillah (Binti yake Mtume), Imam Ali bin Abi Twali (Mumewe) na watoto wao wawili al Hassan na al Hussein, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao. Malipo yao makubwa yametajwa katika sura hiyo ya 76 kuanzia aya ya 10 hadi ya 21.
Ili na sisi malipo yetu yawe makubwa, na futari zetu ziwe na Baraka, ni lazima tutoe vyakula vizuri na tuchunge mwendo mwema katika kuwafuturisha watu.
Mola atujaalie tuwe miongoni mwa wenye kufuturisha. Mola atutaqabbalie vile tunavyovitoa, na atutaqabbalie swaumu zetu, amin Rabbal alamiin.

Ndugu yenu
Ayub Rashid


Somo la 24

Assalam alaikum
Jana tulizungumza kuhusu umuhimu wa kufuturisha na ubora wa sunna hiyo. Ama darsa letu la leo litazungumzia kuhusu wakati wa kula daku, wakati wa sahar na umuhimu wa wakati huu katika kufanya ibada mbali mbali.

Wakati wa kula daku kama tulivyo ona katika darsa zilizopita ni wakati muhimu sana kwa mtu anaefunga. Ni wakati muhimu kwa kuwa huwa tunakula daku, na daku ni sunna ya Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam). Ni wakati muhimu pia kwa sababu huwa tunaswali swala za sunna na kujitayarisha na swala ya alfajiri.

Kuna umuhimu mwingine mkubwa sana unaofungamana na wakati huu wa kula daku, umuhimu mkubwa wa wakati huu ni kusoma dua na pia kufanya istighfaar. Kuna aina nyingi sana za dua za kuombwa na istighfaar nyingi za kuombwa.

Tulisema huko nyuma kuwa wakati wa daku kiarabu unajulikana kama wakati wa sahar na sahar ni wakati kabla ya swala ya alfajiri. Wakati huu una mafungamano makubwa sana na kuomba dua mbali mbali na kufanya istighfaar za kikweli. Huu huwa ni wakati wa utulivu na amani na ni wakati bora wa kumrejelea Mola subhanahu wa taala ili avisikie vilio vyetu.

Katika kuwasifu waumuni wa kweli katika Qur’an, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika sura Adh-Dhaariyaat, sura ya 51, aya ya 15-18;
“Hakika wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchem. Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira”

Ukirejea katika kiarabu aya hizo zinasomeka hivi

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ
آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ
كَانُوا قَلِيلًا مِنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ
وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ

Hapa katika aya hizi Mwenyezi Mungu anawasifu al Muttaqiina, yaani wacha Mungu, na anaonyesha sifa zao na namna gani malipo yao yatakavyokuwa makubwa.

Na kwa kutupendezeshea sifa zao ameanza katika aya ya kumi na tano kwa kuonyesha malipo yao kwa kusema “Hakika wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchem”. Hiyo ni pepo, hiyo ni Janna!

Nini itakuwa hali yao huko? Mwenyezi Mungu anajibu kwa kusema katika aya ya kumi na sita
“Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi”… Hayo ni malipo yao na ni heshima kubwa wanayo heshimiwa na Mola wao.

Kwa nini malipo hayo makubwa watalipwa waumini hawa al Muttaqiina?
“Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema”. Majibu hayo kutoka kwa Mlipaji mzuri. Sasa kufanya mema kunahitajia kujituma, kuna hitajia kuhangaika hapa duniani, kuna hitajia kujinyima! Na ndio Mola anasema
“ Walikuwa wakilala kidogo tu usiku”… Kulala kidogo huku ni kwa sababu ya ibada mbali mbali. Kama vile kuswali, kujifunza masomo mbali mbali, kujisomea na kuyafuatilia mambo ya kheri.
Na amma jambo jingine muhimu watukufu hao walilokuwa wakilifanya ni hili “Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira”.

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ

Sasa zingatia maneno ya kiarabu “wa bil as-haari hum yastaghfiruun”!
As-haar+sahar =wakati au nyakati za kabla ya alfajiri=wakati wa kula daku. Yastaghfiruun+istighfaar=kuomba maghfira=kuomba msamaha kutoka kwa Allah.

Hapa tunajifunza mambo makubwa sana kuwa malipo ya waja wema ambao wameitwa al muttaqiina, yatakuwa makubwa, na hii ni kutokana na wao kufanya mambo mengi mema. Na miongoni mwa mambo hayo ni wao kulala kidogo usiku na kufanya istighafaar na kuomba msamaha kutoka kwa Mola wao.

Hayo mawili ya kulala kidogo usiku na kufanya istighfaar katika kipindi maalum kabla ya swala ya alfajiri, tunaweza kuyafanya katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.

Ikiwa baadhi yetu huweza kukesha kwa kuyafanya mambo mbali mbali yasiyokuwa na umuhimu mkubwa katika maisha yetu hadi alfajiri, ni katika mwezi huu tunaweza kubadilisha muelkeo wetu na kuwa ni watu wenye kulala kidogo na kukithirisha na kufanya kwa wingi istighfaar zetu kwa Mola wetu.

Itakuwa ni vibaya sana sisi kuupoteza wakati wa daku kwa just kungojea kula daku na kisha kwenda kulala. Au kungojea kula daku kwa kutazama sinema na kucheza karata na au siku hizi na kucheza video games na kuchat kwenye simu zetu.
Huu ni wakati wa kuyawacha hayo yote na ku connect na rehema za Allah Mtukufu kwa dua na istighfaar. Huu ni wakati wa ku re-charge betri zetu za imani.

Mola atutaqabbalie istighfaar zetu. Atukubalie msamaha wetu na toba zetu.
Amin Rabbal alamiin

Ndugu yenu
Ayub Rashid

Somo la 25

Assalam alaikum

Katika darsa lililopita tulizungumzia umuhimu wa wakati sahar, wakati wa kula daku. Kama tulivyo ona kuwa kuna aina mbali mbali za umuhimu wa wakati huu ukiwemo ule unaofungamana na kusoma dua na pia kufanya istighfaar.

Na kama tulivyo ona kuwa kuna aina nyingi sana za dua za kuombwa na istighfaar nyingi za kuombwa.

Leo katika darsa letu tuna azimia kuzungumza umuhimu wa istighfaar.
Hebu na tujikumbushe jinsi Mwenyezi Mungu alivyo wasifu waumini wa kweli katika Qur’an, kama alivyo sema katika sura Adh-Dhaariyaat, sura ya 51, aya ya 15-18;

“Hakika wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchem. Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira”

Tumeona katika aya hizo malipo ya waja wema kutoka kwa Mola wetu Mtukufu ambaye Yeye ni mwenye kumsamehe yeyote mwenye kumuomba msamaha wa kweli.

Istighfaar maana yake ni kuomba maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Na maana ya maghfira ni msamaha.

Anaposema mtu ‘astaghfirullah’, maana yake ni kusema naomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Ukimwambie mtu sema ‘astaghfirullah’, maana yake utakuwa umembambia ‘omba msamaha kwa Mwenyezi Mungu’.

Na Mwenyezi Mungu sifa yake ni kukubali msamaha, kwani yeye ni al Ghafuur, maana yake ni Mwenye kusamehe sana, ingawaje anaweza kuadhibu.
Na ni bora Tukasema kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kusamehe, Mwingi wa kusamehe na daima husamehe pindi anapo ombwa msamaha kwa dhati.

Husamehe kwa mapenzi yake, ingawaje akiamua kuadhibu basi ni mkali sana wa kuadhibu!

Tunakuta sifa zake za kusamehe katika Qur’an kuwa Yeye Allah sio tu ni al Ghafuur, Mwingi wa kusamehe, bali sifa yake hiyo huambatana na sifa nyingine, kwa mfano;

Al Ghafuur ar Rahiim,
Al Aziiz al Ghafuur
na Al Ghafuur al Waduud

Yeye ni al Ghafuur ar Rahiim, kama ilivyo katika sura al Qaswas, sura ya 28 aya ya 16, na pia sehemu nyingi katika Qur’an

“hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu”

Pia Allah ni al Aziiz al Ghafuur, kama alivyo sema katika sura al Mulk, sura 67 aya ya 2, “Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha”

Na pia Mola wetu ni al Ghafuur al Waduud, kama ilivyo katika sura al Buruuj, sura ya 85 aya ya 14,
“Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi”

Endapo tutakaa katika wakati wa sahar na kumuomba Mola wetu atusamehe dhambi zetu, na tukamuomba kwa dhati, kwa lugha yeyote ile, basi tujue Mola wetu Mlezi atausamehe dhambi zetu.

Na masha Allah, dini ya Kiislamu ni dini nzuri sana, endapo wewe umemkosea Mola wako, huna haja ya kwenda kuungama na kutoa siri zako kwa mtu mwingine ili yeye akuombee msamaha kwa Mola wako. Unachotakiwa ni kutokutoa siri yako hiyo, bali ukae umuelekee Mola wako kwa nia safi ya kumuomba msamaha, na Yeye atakuwa ni mwenye kusikia istighfaar na msamaha wako. Kwa sababu Mola ni Mola wako, si Mola wa mwenzako tu!

Mola wetu anasema katika sura an Nisaa, sura ya nne, aya ya 110

وَمَنْ يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّهَ يَجِدِ اللَّهَ غَفُورًا رَحِيمًا

“Na anaye tenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghfira kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu”

Somo hili la istighfaar ni pana sana, kwani lina umuhimu mkubwa sana, na moja ya faida zake ni kuwa msamaha wetu ukikubaliwa, huwa ndio tumepewa ukurasa mpya msafi wa sisi kuanza maisha yetu upya.
Na ni hapo ndipo tunapo mshinda sheitwani na mbinu zake za kutaka kuturudisha nyuma katika madhambi.

Mwezi wa Ramadhan unajulikana kama mwezi wa Istighfaar, na hakuna wakati bora kama wakati wa daku, wakati wa sahar, huu ndio wakati wa sisi kukaa na kumlilia Mola wetu Mlezi ili atusamehe dhambi zetu. Dhambi za aina yoyote ile, na hata ziwe ni dhambi ndefu na zenye ukubwa kama mlima Kilimanjaro, Mola wetu tukimuomba msamaha wa kweli, Mola wetu Mlezi atatusamehe dhambi hizo.

Kesho tutaendelea na sehemu ya mwisho ya darsa hili, insha Allah.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atukubalie misamaha yetu. Atupe fursa ya kumuomba kwa dhati. Atujaalie tuya anze maisha yetu upya katika mwezi huu wa Ramadhan.

Ndugu yenu
Ayub Rashid


Somo la 26

Assalam alaikum

Katika darsa lililopita tulizungumzia umuhimu wa istighfaar. Na leo insha Allah tuna azimia kukamilisha mada hii pana na yenye umuhimu mkubwa, bila shaka tumeyawacha mengi yenye faida, na hii ni kutokana na ufinyu wa nafasi na muda.

Katika darsa hili tunataka kutazama faida za aina mbili zinazo patikana kwa kumuomba Allah msamaha.
Faida hizi tutazigawanya katika makundi au sehemu mbili;

1. Faida za kiroho 2. Faida za kimwili.

Faida za kiroho
Ama faida za kiroho tunaziona pale mtu anapomuomba Mola wake msamaha, na akaamini kuwa Mola wake amemsamehe, utamuona mja huyo kuwa ni mwenye bashasha na furaha na moyo wake unakuwa umetulia.
Mja hujihisi kama aliye tuliwa mzigo mzito aliokuwa ameubeba katika kichwa chake.

Faida hii ya kiroho ni muhimu sana kwani humfanya mtu awe na utulivu moyoni mwake. Na hii ni power kubwa na nguvu isiyomithilika ya istighfaar.

Na endapo utalitazama swala hili kinyume, ukamuona mtu ambae amemuasi sana Mola wake, au amefanya dhambi kubwa, hata kama hajamwambia mtu na kumfichulia dhambi hiyo, na akawa mtu huyo hajamuomba Mola wake istighfaar na msamaha wa kweli, na au akawa anaamini kuwa hata kama atamumba Mola wake hatosamehewa, mtu huyu huwa anaishi katika hali ya kukosa raha, huwa mgomvi na aliyekata matumaini.

Hii ni athari mbaya sana ya kiroho inayoletwa na kukata tama ya kuto kusamehewa.

Hebu na tuirejelee Qur’an tuone inasema nini kuhusu kukata tama baada ya kufanya madhambi.

Allah Mtukufu anasema katika sura az-Zumar, sura ya 39,aya ya 53

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِنْ رَحْمَةِ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

“Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu”

Ni wazi kuwa Mwenyezi Mungu Mlezi anatupa moyo wa kutokukata tamaa pindi tunapomuasi, kwani Yeye husamehe dhambi zote.

Na ni vizuri sana tukawa na sisi ni wenye kupeana moyo wa kuanza ukurasa mpya baada ya kutubia madhambi tuyafanyayo, badala ya kukatishana tamaa na kuwa sisi ndio kama-astaghfirullah-ndio miungu watu!

Naam, ni kweli kuwa kuna dhambi ambayo Mwenyewe Mwenyezi Mungu hatoisamehe, nayo ni ya kumshirikisha Allah, na kumfanyia kuwa anae mwenzake kama Yeye.
Endapo mtu ataifanya dhambi hii kwa kujua, na akafa katika ibada hiyo ya shirki, huyo hatosamehewa, kwa kuwa amefanya dhulma kubwa sana.
Na hayo ni kwa mujibu wa Qur’an tukufu, sura an Nisaa, sura ya nne, aya ya 48

“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa”

Faida za kimwili
Ama faida za kimwili za istighfaar ni nyingi sana, wacha tuziorodheshe kwa mujibu wa Qur’an.

Na tuirejelee sura Nuhu,sura ya 71, aya ya 10-12.

فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا
يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُمْ مِدْرَارًا
وَيُمْدِدْكُمْ بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَلْ لَكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَلْ لَكُمْ أَنْهَارًا

“ Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe. Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo. Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito”

Hapa katika aya hizo tatu muhimu, nabii Nuhu (alaihi wa alaa Nabiyyinas salaam) anawafunuliwa na kuwa onyesha watu wake faida za kimwili za istighfaar kwa kuwaambia kuwa endapo watamuomba Mola wao msamaha wa kweli kweli watapatiwa mambo yafuatayo;

1. Mvua zenye kuendelea, na hizi zitastawisha mazao, kisha watavuna
2. Watapata mali nyingi na zenye Baraka
3. Watajaaliwa watoto
4. Wataruzukiwa mabustani
5. Watapatiwa pia mito ya maji, na hii italeta neema nyingi

Ukijiuliza hayo yatawezekanaje kupatikana kwa kufanya istighfaar tu peke yake?

Ndipo Tukasema pale mwanzo kuwa, kumuomba msamaha wa kweli kunatupatia faida kubwa mbili, nazo ni za kiroho na kimwili. Kwani Yule tunaeomba msamaha kwake Yeye ndiye Mmiliki wa kweli wa vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.

Ni kwa istighfaar zetu basi Mola wetu Mlezi atatufungulia hazina za hii dunia, ili tuweze kujitosheleza na kumuabudu Yeye katika wasaa na ukunjufu wa mwili na roho.

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa istighfaar, basi na tukithirishe kumuomba Allah msamaha kwa makosa yetu yote tuliyoyafanya ili tuanze tena upya maisha ya kuwa huru kutokana na madhila ya madhambi.

Astafhfirullah, astaghfirullah, astaghfirullah

Astaghfiru Allah Rabbi wa atuubu ilayhi, namuomba Allah Mola wangu msamaha na natubia kwake.

Ndugu yenu
Ayub Rashid


Somo la 27

Assalam alaikum

Darsa letu la leo litatazama na kuzungumzia kuhusu zaka kwa ujumla na zakatul fitra khasa. Tutanza insha Allah kwa kutazama maana ya zakatul fitra. Tutaeleza aina za zaka. Umuhimu wa zaka hii, anaetakiwa kutoa, nani anaestahiki kupewa na nini faida za mtoaji na Yule anayepokea.

Utangulizi

Zaka ni moja ya nguzo muhimu za maswala ya kiuchumi katika Uisilamu. Dini hii tukufu haikuliwacha swala la kiuchumi kama hili bila ya kulizungumzia na kulielekeza namna ya kulitekeleza kwake. Ni jambo la hakika, Ikiwa zaka itatolewa kama alivyo amrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakutobaki fakiri wala masikini katika jamii nyingi za waisilamu.

Maana ya zaka

Neno zaka lina maanisha kutakasa, na pia lina maana ya kukua na kuongezeka. Neno hili likiambatanishwa na mali anayoitoa mtu basi litafahamika kuwa zaka ni seehemu ya mali anayoitoa mtu ili aitakase mali yake na aifanye ikue na kuongezeka. Endapo mtu hatoitolea mali yake zaka, basi itakuwa mali hiyo bado ni chafu na itakosa baraka ya Mwenyezi Mungu.

Aina za zaka

Kuna aina mbili kubwa za zaka katika dini ya Kiislamu. Zaka ya kwanza ni ile inayojulikana kama zakatul maal, au zaka ya kutoa kila mwaka sehemu ya mali mtu aliyokuwa nayo, ili kuwapatia wale wanaostahiki. Zaka ya pili ni ile zakatul fitra. Hii ni zaka inayotolewa baada ya kukamilisha funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Zaka hii hutolewa usiku wa kuamkia siku ya Eid al Fitr, au hutolewa asubuhi ya siku ya sikukuu ya Eid al Fitr.

Umuhimu wa zaka

Uisilamu umeipa kipa umbele kikubwa ibada ya zaka kwa ujumla. Utaona katika sehemu nyingi sana katika Qur’an tukufu, Mwenyezi Mungu anapotaja kuhusu kusimamisha swala, ataongeza na kutoa zaka.

Kwa mfano tu, Mwenyezi Mungu anasema katika sura an Naml, sura ya 27, aya ya 3, kama ifuatavyo;
“Ambao wana simamisha Swala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini nayo”

Pia Mwenyezi Mungu katika Qur’ani tukufu, sura al Mu’minuun, sura ya 27 aya ya nne, katika kuwasifu waumini anasema kuwa;

“na ambao wanatoa zaka”. وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ

Na kuna Hadith nyingi za bwana Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam) zinazo onyesha umuhimu wa kutoa zaka.

Uisilamu umeifanya zaka kuwa ni wajibu wakila mwenye uwezo kutoa, ili wale walio nacho wawapatie wale wasio nacho.

Zakatul Fitra.

Zaka hii huwa ikitolewa mara moja katika mwaka. Imeitwa zakatul fitra kwa sababu hutolewa usiku wa kuamkia Eid al Fitr au asubuhi ya siku hiyo. Na Eid hii huja baada ya kukamilisha swaumu ya mwezi Mtukufu wa Ramdhan.

Ni lazima kwa kila mtu mwenye uwezo kuitoa zaka hii na kuwapatia wale wasiokuwa na uwezo. Na kila mtu ambae anasimamia familia yake, ni lazmia atoe zaka yake na ya watu wake wote wa familia yake na wale wanaomtegemea yeye, kama baba na mama walio watu wazima.

Nini kinachotolewa?

Kila mtu atatakiwa atoe zakatul fitra yake kiwango cha takriban kilo tatu za chakula maarufu kinacholiwa katika mji anaoishi, na kilo tatu hizo zitapewa Yule anaestahiki. Mtoaji anaweza kutoa chakula au atoe pesa zinazo lingana na bei ya chakula hicho.

Wanao toa na wanao stahiki kupewa
Mtoaji wa zakatul Fitra ni lazima awe muisilamu, mwenye uwezo, mwenye akili na awe ni mtu mzima.

Ama anaestahiki kupewa ni lazima awe;

1. Muislamu, ambae ni masikini au fakiri au mtu mwenye kuhitajia.
2. Ni muhimu kumpatia mtu ambae ni mshika dini.
3. Pia anafaa kupewa muisilamu aliyezongwa na madeni ambae hawezi kulipa madeni yake kutokana na umasikini.
4. Waisilamu wanao pita kukusanya zaka na kuisambaza.
5. Msafiri aliyekwama njiani na ameishiwa pesa za safari

Masharifu na wasio kuwa masharifu
Katika jamii zetu tunazoishi, wapo watu miongoni mwetu wanaoitwa masharifu au masayyid. Hawa ni wale waisilamu ambao nasaba zao zinarudi hadi katika ukoo wa Mtume Muhammad (swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam).
Masharifu kwa kawaida huwa hawapokei zaka, kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume Muhammad (saww). Ama katika swala la zakatul Fitra, wana ruhusiwa kupewa zaka hii, lakini wapewe na masharifu wenzao. Zakatul fitra ya sharifu itakwenda kwa sharifu mwenzake mwenye kustahiki. Na hairuhusiwi kinyume cha hivyo.

Wakati wa kutoa zakatul fitra

Zaka hii hutolewa usiku wa kuamkia siku ya Eid, au asubuhi ya siku ya Eid, kama tulivyo tangulia kusema. Endapo mtu ataitoa zaka hii kabla ya nyakati hizo mbili haitohesabiwa kama ni zakatul Fitra.

Lakini, endapo mtu ataamua kumpatia mwingine pesa kama amana, au deni, ili azitoe siku ya Eid kama zakatul Fitra, hapo atakuwa amefanya sawa sawa. Kwa hivyo watu waliokuwa mbali na miji yao, wanaweza kuzituma pesa zao kabla ya siku ya Eid, pesa hizo zihifadhiwe ili zitolewe kama zakatul Fitra na kupewa wale wanao stahiki.

Ndugu na jamaa wa karibu

Ni vizuri kuchunga watu kuwapatia zakatul Fitra, kuanza kwa kuwapa ndugu na jamaa wa karibu katika familia. Kama wamo watu miongoni mwa familia zetu wanaostahiki kupewa, basi na tuwape wao kwanza kabla hatujatoka nje ya familia zetu.

Faida kwa mtoaji na mpokeaji

Tukianza na mtoaji, pindi mtu anapotoa zakatul Fitra yake huwa ameifanya swaumu yake imefika kwa Mola wake. Kwani kama hatotoa zaka hii, mfungaji wa mwezi wa Ramadhan, swaumu yake itakuwa inaelea kati ya dunia na mbinguni. Vile vile zakatul Fitra humuokoa mtoaji na mabalaa mengi. Na mwisho humfanya awe ameridhiwa na Mola wake kwa kutekeleza ibada muhinu sana ya kuitakasa mali yake.
Ama faida kwa wapokeaji, siku ya Eid ni siku ya furaha ambayo husherehekewa na waisilamu duniani.
Mafakiri na masikini wetu huwa wanataabika kutafuta riziki zao kila siku na hivyo kukosa raha katika maisha yao. Endapo watapatiwa zakatul Fitra katika mapema ya siku ya Eid, hilo litawafanya na wao pia waisherehekee sikuu ya Eid kwa furaha kubwa.
Na furaha hii huwa ni kwao na kwa jamii yao. Furaha hii huwa ina enea na kusambaa katika jamii yetu na kuifanya siku ya Eid iwe ni siku special kwa kila mtu.

Mbali na kuwa mpokeaji huwa na furaha katika siku ya Eid al Fitr, bali huwa pia akimuombea Yule aliyetoa na kumshukuru Mola wake kwa kumpatia neema zake katika siku hii muhimu baada ya kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kutoa fitra zetu. Mola atautaqabbalie zaka zetu. Awatoe katika tabu na madhila mafakiri na masikini wetu.

Ndugu yenu
Ayub Rashid

WRITTEN BY: abu@tapsw

No comments yet.

Leave a reply

Reset all fields